21-02-2026 07:52:49
•
KCMC-UBONGO
•
2 min read
WATU 6 WANUFAIKA NA NJIA ZA KISASA ZA KUTIBU VIVIMBE VYA UBONGO
Madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu wenye ubobezi katika kutibu vivimbe vya ubongo kutoka University of Colorado nchini Marekani, wameweka kambi maalum ya siku mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini - KCMC.
Kambi hiyo ya kibingwa imefanyika kwa ushirikiano kati ya madaktari hao wa kimataifa na madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na wataalamu wa upasuaji wa sakafu ya fuvu (skull base surgery) kutoka KCMC. Lengo kuu la kambi hii limekuwa kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wenye vivimbe vya ubongo, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu.
Kwa siku mbili, jumla ya wagonjwa sita wenye vivimbe vya ubongo wamefanyiwa upasuaji na upasuaji huo ulifanyika kwa njia ya kupitia puani, huku nyingine ikifanyika kupitia juu ya fuvu, kulingana na aina na eneo la uvimbe. Mbinu hizi hupunguza muda wa kulazwa hospitalini, na kuongeza uwezekano wa kupona kwa haraka.
Upasuaji huo ulifanyika kwa msaada wa vifaa maalumu vya kisasa ikiwemo hadubini za upasuaji (surgical microscopes) na kamera maalumu za endoscope, zinazowezesha madaktari kuona kwa uwazi mkubwa maeneo yenye changamoto ndani ya ubongo bila kufanya upasuaji mkubwa unaoweza kuongeza hatari kwa mgonjwa.
Ujio wa madaktari hao ni mwanzo rasmi wa ushirikiano wa kimkakati wa kiutendaji kati ya University of Colorado na hospitali ya KCMC.
Related News