Taasisi ya Shirika la Msamaria Mwema · Moshi
🫀 Taarifa kwa Umma · 09 Aprili 2026
Uchangiaji wa Ujenzi wa Jengo
la Matibabu ya Moyo
KILIMANJARO CHRISTIAN MEDICAL CENTRE – KCMC
TSh 50B
Gharama Zote za Mradi
90%
Ufadhili wa Kimataifa
24,585
Wagonjwa wa Moyo (2020–2025)
102
Vitanda vya Wagonjwa
Kilimanjaro Christian Medical Centre – KCMC
Kilimanjaro Christian Medical Centre – KCMC ni hospitali ya Rufaa ya Kanda inayotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi (consultant and referral specialized hospital) iliyoanzishwa tarehe 06 Machi, 1971 ikihudumia wananchi wa Kanda ya Kaskazini ya Tanzania, inayojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Hospitali hii ipo Mkoa wa Kilimanjaro lakini inahudumu wahitaji hata kutoka nje ya mipaka ya eneo lake la rufaa. Kwa zaidi ya miaka 50, KCMC imekuwa nguzo kuu ya afya kwa wananchi wa Tanzania kaskazini na zaidi.
KCMC – Tangu 06 Machi, 1971
Taasisi ya Shirika la Msamaria Mwema · Moshi
KCMC – Moshi, Kilimanjaro, Tanzania
Magonjwa ya Moyo Kimataifa
Magonjwa yasiyoambukiza (Non-communicable diseases – NCDs) kwa sasa yanachangia takribani asilimia 70 ya vifo duniani. Miongoni mwa magonjwa haya, magonjwa ya moyo na mishipa (cardiovascular diseases – CVDs) ndiyo chanzo kikuu cha vifo.
Magonjwa kama Kiharusi (stroke) na ugonjwa wa kuziba kwa mishipa ya moyo (ischemic heart disease) yanachangia sehemu kubwa ya vifo hivi. Zaidi ya asilimia 78 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Tofauti na nchi zilizoendelea, katika nchi hizi magonjwa ya moyo huanza kuathiri watu wakiwa katika umri mdogo, hali inayopunguza nguvu kazi na kuathiri maendeleo ya kiuchumi.
70%
Vifo vya NCDs Duniani
78%
Vifo vya NCDs – Nchi Maskini
Magonjwa ya Moyo Hospitali ya KCMC
Magonjwa ya moyo ni miongoni mwa sababu kuu za wagonjwa kulazwa KCMC. Takwimu za hospitali zinaonyesha kuwa asilimia 14.4 ya wagonjwa wanaolazwa ni wagonjwa wa moyo, ambao hulazwa hospitalini kwa wastani wa siku 9 hadi 10. Asilimia 38.5 ya wagonjwa wanaoruhusiwa hulazwa tena baada ya muda.
Kiwango cha vifo kwa wagonjwa wa moyo ni takribani asilimia 18.3 ya vifo vyote vinavyotokea KCMC. Katika kipindi cha miaka mitano (2020–2025), jumla ya wagonjwa 24,585 kati ya 135,136 waliolazwa walikuwa na magonjwa ya moyo.
Aidha, zaidi ya wagonjwa 133,000 kati ya 1,502,236 wa nje walipatiwa huduma za matibabu ya moyo katika kipindi hicho. Hii ni ishara ya ongezeko kubwa la magonjwa ya moyo nchini Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni.
14.4%
Wagonjwa wa Moyo wanaolazwa
18.3%
Vifo vya Wagonjwa wa Moyo
24,585
Wagonjwa wa Moyo (2020–2025)
133,000+
Wagonjwa wa Nje (2020–2025)
Lengo Kuu la Mradi
Katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya moyo nchini na kuboresha huduma za kibingwa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini – KCMC imeanzisha mpango maalum unaojumuisha wazo la kuboresha huduma za moyo, ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha kliniki ya moyo.
🎯 Lengo Kuu
Kuanzisha Kituo cha kisasa cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa (fully functional Cardiovascular Centre) katika hospitali ya KCMC kitakachotoa huduma kamili za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa moyo kwa Kanda ya Kaskazini ya Tanzania na maeneo mengine ndani na nje ya nchi.
💡 "Kuwa jukumu la Afya sio la Serikali tu. Hiyo ndo maana KCMC inataka kuanza huduma hii."
Mfano wa 3D wa Jengo la Cardiovascular Centre
Malengo Mahususi ya Kituo
Kituo kipya cha Matibabu ya Moyo kitalenga maeneo mbalimbali ya huduma ili kuhakikisha Watanzania wanapata matibabu kamili ya moyo ndani ya nchi yao, na hivyo kupunguza hitaji la rufaa za nje ya nchi.
- ✦ Kuimarisha kinga, kutoa elimu kwa jamii na uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya moyo
- ✦ Kuanzisha huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu ya moyo
- ✦ Kutoa matibabu ya dawa, matibabu ya kutumia mirija maalum (catheter-based treatment) na upasuaji wa moyo (cardiac surgery)
- ✦ Kutoa huduma za urekebishaji wa afya ya moyo (cardiac rehabilitation) pamoja na ufuatiliaji wa muda mrefu
- ✦ Kupunguza uhitaji wa rufaa za nje ya nchi na mzigo kwa taasisi pekee iliyopo Tanzania
Jengo la Ghorofa Tatu la Kisasa
Kitengo hiki kitakapokamilika kitakuwa na jengo la kisasa lenye ghorofa tatu litakalojumuisha vyumba na vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo.
Gharama za Mradi na Ushirikiano wa Kimataifa
Ujenzi wa jengo utagharimu shilingi bilioni 25 za Kitanzania, na vifaa tiba na vifaa vya hospitali vitagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 25 za Kitanzania — jumla ya shilingi bilioni 50 kwa mradi wote.
Wataalamu watakaohudumia kitengo hiki wanapata mafunzo yao nchini India na Tanzania na wanapata ufadhili kutoka kwa mdau aitwae Global Heartcare Foundation.
🌍 Ushirikiano wa Kimataifa
KCMC tayari imeingia makubaliano ya ushirikiano na wadau wa kimataifa ambao wamekubali kufadhili asilimia 90 ya gharama za ujenzi. Msaada wa Watanzania wenyewe unakamilisha asilimia iliyobaki ya mradi huu wa kihistoria.
TSh 25B
Gharama za Ujenzi
TSh 25B
Gharama za Vifaa
KCMC – Ujenzi na Ushirikiano wa Kimataifa
Rai kwa Watanzania Wote — Ndani na Nje ya Nchi
Kupitia vyombo vya habari, tunatoa wito wa dhati kwa Watanzania wote popote mlipo ndani ya mipaka ya nchi yetu na nje ya nchi kuungana katika juhudi hii ya kitaifa. Huu si mradi wa KCMC pekee. Huu ni mradi wa Watanzania wote.
Ni mradi wa kulinda maisha ya ndugu zetu, wazazi wetu, watoto wetu, na vizazi vijavyo. Tunawaomba Watanzania wa kila rika na kila nafasi — vijana, wazee, wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima, viongozi, na diaspora yetu kuchangia kwa moyo wa uzalendo na mshikamano.
Kila mchango ni muhimu.
Kila mchango ni uhai.
Kila mchango ni tumaini.
"Kwa pamoja, tunaweza kujenga kituo hiki.
Kwa pamoja, tunaweza kuokoa maisha."
JINSI YA KUCHANGIA
Ndugu Watanzania, Unaweza kuchangia kupitia njia zifuatazo.
Hakikisha jina la akaunti ni:
KCMC MOYO
Akaunti za Benki
Namba ya Akaunti
Namba ya Akaunti
Namba ya Akaunti
Namba ya Akaunti
Mitandao ya Simu
Lipa Namba
Namba ya Wakala
Nje ya Mtandao
Mchango Ana kwa Ana
Mnakaribishwa kufika moja kwa moja katika hospitali yetu kwa msaada wa karibu.
Hospitali ya KCMC, Moshi
Tunawapokea kwa heshima kubwa
Uongozi wa Hospitali
KCMC – Kilimanjaro
Taasisi ya Shirika la Msamaria Mwema
Dar es Salaam, 09 Aprili 2026
Tuchangie Leo. Tuokoe Maisha Kesho!
Kwa pamoja, tunaweza kujenga kituo hiki.
Kwa pamoja, tunaweza kuokoa maisha.
Na kwa pamoja, tunaweza kuandika historia mpya ya huduma za afya nchini Tanzania.
Mchango wako unalindwa na uhakika wa KCMC — Taasisi ya Shirika la Msamaria Mwema, Moshi.