17-02-2026 13:22:50
•
KCMC
•
4 min read
CPA. ELLEN MGOJI: INTERNET BANKING NI HITAJI, SIO CHAGUO TENA
Moshi, Februari 17, 2026 — Taasisi za sekta binafsi na umma zimehimizwa kukumbatia kikamilifu matumizi ya teknolojia ya kifedha ili kuongeza ufanisi, uwazi na ushindani katika utoaji wa huduma. Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa Hospitali ya KCMC, CPA Ellen Mgoji, alipokuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la Elimu ya Huduma za Benki kwa njia ya Internet Banking lililoandaliwa na CRDB Bank na kufanyika katika Ukumbi wa Kuringe Social Hall, Moshi.
Akizungumza mbele ya viongozi wa taasisi mbalimbali, wawakilishi wa sekta binafsi na umma pamoja na waandishi wa habari, CPA Mgoji alisisitiza kuwa katika dunia ya sasa, teknolojia si chaguo bali ni hitaji la lazima kwa taasisi zinazotaka kuendelea kuwa imara na zenye ushindani.
“Matumizi ya Internet Banking yamerahisisha kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa shughuli za kifedha katika taasisi zetu. Yamepunguza muda wa miamala, gharama za uendeshaji na hatari zinazoweza kujitokeza katika utunzaji wa fedha taslimu,” alieleza CPA Mgoji.
Kwa mujibu wake, katika sekta ya afya hususan, mifumo ya kidijitali imekuwa msaada mkubwa katika usimamizi wa rasilimali fedha, malipo ya watoa huduma, ununuzi wa vifaa tiba na ukusanyaji wa mapato. Alibainisha kuwa upatikanaji wa taarifa za kifedha kwa wakati halisi unaongeza uwajibikaji na kuwezesha maamuzi ya haraka na sahihi.
Akizungumzia mageuzi ya sekta ya benki, alisema kuwa kupitia uwekezaji mkubwa katika TEHAMA, taasisi za kifedha zimeweza kuleta huduma salama, rahisi na zenye kuaminika zaidi. Alitaja faida za Internet Banking kuwa ni pamoja na kurahisisha malipo ya mishahara, kulipa wazabuni na wasambazaji kwa wakati, kufuatilia miamala muda wowote na kupunguza matumizi ya hundi na fedha taslimu.
“Huduma hizi zinaimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha za taasisi,” aliongeza.
CPA Mgoji aliipongeza CRDB Bank kwa kuandaa kongamano hilo la elimu, akisema kuwa teknolojia bila uelewa sahihi kwa watumiaji haiwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Alihimiza taasisi zote kuhakikisha zinatumia kikamilifu mifumo ya kisasa ya kibenki ili kuongeza ushindani na kuboresha utendaji.
Related News