2026-04-22 00:00:00
•
MAADHIMISHO
•
5 min read
WIKI YA MAABARA YAIBUA MJADALA MUHIMU
Ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Wataalamu wa Maabara za Afya Duniani, wataalamu wa afya wamepata fursa adhimu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kutoka kwa wataalamu wa maabara kupitia kongamano la afya lililofanyika leo Aprili 22, 2026 katika ukumbi wa maktaba KCMC.
Kongamano hili limeongozwa na Prof. Ireen Kiwelu, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara, ambaye aliwasilisha mada muhimu kuhusu maendeleo ya maabara na mchango wake katika kuboresha huduma za afya. Kupitia wasilisho lake, alieleza kuwa KCMC ipo hatua za mwisho za kukamilisha jengo na ufungaji wa vifaa (Centre of Excellence Laboratory), kituo kitakachoboreshwa kwa teknolojia ya kisasa ili kuimarisha huduma za uchunguzi, utafiti na mafunzo. Alisisitiza kuwa uwekezaji huu utapunguza muda wa majibu ya vipimo, kuongeza usahihi wa uchunguzi na kuwezesha wagonjwa kupata huduma bora kwa wakati.
Aidha, Prof. Balthazar Nyombi aliwasilisha mada kuhusu mabadiliko ya huduma za maabara nchini Tanzania, akibainisha safari ya maendeleo kuanzia enzi za ukoloni hadi mfumo wa kisasa unaozingatia ubora, usalama na viwango vya kimataifa kama ISO 15189. Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya maamuzi ya kitabibu hutegemea majibu ya maabara, jambo linaloonesha umuhimu mkubwa wa wataalamu hawa katika mfumo mzima wa huduma za afya.
Kwa upande wake, Saniru Bia Kimweri alieleza kwa kina nafasi ya maabara katika tiba, akisisitiza kuwa maabara ni msingi wa utambuzi sahihi wa magonjwa, mwongozo wa matibabu stahiki pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya mgonjwa. Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wataalamu wa maabara, madaktari na wataalamu wa radiolojia huongeza ubora wa huduma na kuokoa maisha.
Kongamano hili limekuwa jukwaa muhimu la kuongeza uelewa kuhusu mchango mkubwa wa wataalamu wa maabara katika sekta ya afya, huku likihamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa, utafiti na ubunifu ili kuboresha huduma kwa jamii.
#LabWeek2026 #MedicalLaboratoryProfessionals #KCMC #AfyaKwanza #healthcareexcellence
Related News