KCMC NA HOPE MOBILITY WALETA TABASAMU KWA WATU 300+
Leo, tarehe 19 Oktoba 2026, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini -KCMC kwa kushirikiana na Hope Mobility kutoka Kenya na Marekani (USA), imeendesha zoezi la ugawaji wa viti mwendo kwa watu wenye uhitaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha maisha ya watu wenye changamoto za utembeaji na kuwawezesha kujitegemea katika shughuli zao za kila siku.
Zoezi hilo limeongozwa na Bw. Michael Panther, mwanzilishi wa Hope Mobility Kenya, ambaye ameshiriki katika kuendeleza juhudi za kuhakikisha watu wenye changamoto za utembeaji wanapata vifaa saidizi vinavyowawezesha kuishi maisha yenye utu na kujitegemea.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Prof. Gileard Masenga, ametoa shukrani zake za dhati kwa Hope Mobility kutoka Kenya na Marekani kwa mchango wao na ushirikiano wao katika kufanikisha zoezi hilo. Amesema kuwa mchango huo una umuhimu mkubwa katika kuwasaidia watu wenye changamoto za utembeaji kupata fursa ya kujitegemea, kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kijamii na kuboresha maisha yao.
Zoezi hilo linaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za afya na wadau wa maendeleo katika kuboresha ustawi wa jamii, hususan kwa watu wenye mahitaji maalumu, kwa kuhakikisha wanapata vifaa saidizi vinavyowasaidia kukabiliana na changamoto za utembeaji na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.
KCMC inaendelea kuthamini ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya na kuboresha maisha ya jamii.
Related Stories
2026-10-16 00:00:00