UJENZI WA WODI ZA TIBA YA MAGONJWA YA MFUMO WA FAHAMU WAANZA
Hospitali ya KCMC yaanza rasmi hatua za ujenzi wa jengo la Wodi za Tiba ya Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu, kupitia sala maalumu iliyofanyika leo tarehe 13 Oktoba 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard G. Masenga, amesema mradi huo unaakisi dhamira ya KCMC ya kuendelea kutoa huduma bora za afya zinazomweka mgonjwa mbele, pamoja na kuimarisha mafunzo na utafiti kwa kuzingatia upendo wa Kristo.
Prof. Masenga ameeleza kuwa magonjwa ya mfumo wa fahamu, yakiwemo kiharusi, kifafa, uvimbe wa ubongo na majeraha ya uti wa mgongo, yanahitaji huduma za haraka na za kibingwa. Hata hivyo, amesema kutokuwepo kwa wodi maalumu kwa wagonjwa hao katika KCMC kumekuwa changamoto katika utoaji wa huduma na ufuatiliaji wa matibabu yao.
Amesema jengo linalotarajiwa kujengwa litakuwa na uwezo wa vitanda 40 na linatarajiwa kuhudumia hadi wagonjwa 14,600 kwa mwaka. Aidha, jengo hilo litakuwa na huduma muhimu zitakazojumuisha famasia, vyumba vya uangalizi wa wagonjwa, vyumba vya kubadilishia mavazi kwa watumishi pamoja na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma.
Katika hotuba yake, Prof. Masenga ametoa shukrani kwa wadau wa maendeleo, hususan Fidesco Netherlands na Wilde Ganzen Foundation, kwa msaada wao wa kifedha uliowezesha mradi huo kufikia hatua ya kuanza. Pia amempongeza Dkt. Marieke Dekker kwa kujitoa kwake na mchango wake muhimu katika kufanikisha mpango huo.
Vilevile, ameitambua Menejimenti ya KCMC, Idara ya Mipango na Miradi, timu za kliniki, Idara ya Uhandisi pamoja na watumishi wengine walioshiriki katika maandalizi na uratibu wa mradi huo.
Akisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mradi, Prof. Masenga amesema mafanikio yake hayatapimwa kwa kukamilika kwa jengo pekee, bali pia kwa maisha yatakayookolewa, wagonjwa watakaohudumiwa na kuongezeka kwa ubora wa huduma za afya zitakazotolewa.
Ameongeza kuwa KCMC itaendelea kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi, kwa kuzingatia uwajibikaji wa kifedha, viwango vya ubora na uratibu madhubuti katika kila hatua ya utekelezaji.
Related Stories